Dar es Salaam. Shirika la Umeme (Tanesco) limesema limbikizo la deni la Sh275 bilioni kwa taasisi mbalimbali za Serikali na wateja binafsi, linachangia kukwamisha utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Hata hivyo, Tanesco imeelezwa kuwa deni hilo limeanza kupunguzwa na mpaka kufikia Juni, mwaka huu, takriban Sh30 bilioni zilikwishalipwa na wadaiwa.
Kutokana na ukosefu wa fedha, Tanesco inafanya juhudi za ziada ili kufanyia matengenezo transfoma inayosambaza umeme katika eneo kubwa la Kipawa jijini.
Akizungumza jana na gazeti hili, msemaji wa shirika hilo, Adrian Severin alisema hutamani kufanya kazi bila kuwakera wateja wao, lakini tatizo la fedha linawafanya washindwe kufikia malengo.
Hata hivyo, Severin alisema baada ya kufikia kikomo cha muda wa tangazo la ukusanyaji wa madeni hayo, Tanesco itaanza kuchukua hatua kali dhidi ya wadaiwa wote sugu.
“Kuna ripoti ambayo tutaipokea leo (jana) itakayokuwa na mwelekeo wa jinsi gani tutakusanya madeni hayo. Inasikitisha kuona taasisi za Serikali na wateja wengine hawalipi madeni yao wakati wanaendelea kupata huduma,” alisema.
“Shirika linaathirika sana na deni hilo, tunashindwa kutoa huduma kwa ufanisi katika maeneo mengi kwa sababu ya kukosa fedha. Kiasi hicho kama kingekuwapo kingeweza kusaidia kutatua changamoto hizi ambazo kwa kweli ni kero kubwa kwa wateja wengine.”
Akizungumzia transfoma ya Kipawa, Severin alisema mainjinia wa Tanesco wamebaini tatizo kubwa ambalo litatatuliwa baada ya siku tatu mpaka nne.
“Kuna mtaalamu atafika leo (tangu jana) kutoka India kwa ajili ya kuitengeneza. Inaweza kukamilika Jumatano au Alhamisi,” alisema alisema Severin.
Alisema kuharibika kwa transfoma hiyo, kumeyafanya maeneo ya Kisarawe, Gongo la Mboto, Kivule, Kipunguni, Ukonga, Tabata, Uwanja wa Ndege, Chang’ombe, Tandika, Nyerere Road na maeneo jirani kukosa umeme.
Alisema ili kupunguza usumbufu, umeme unaotumiwa katika makazi ya watu kwa sasa utatoka katika transfoma ya Ubungo, “lakini kwa viwanda itabidi wasubiri mpaka matengenezo yatapokamilika.”
Na Kelvin Matandiko na Daula Abdul, Mwananchi
0 comments:
Post a Comment